Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Keating akaribisha tathimini ya sheria ya vyombo vya habari Somalia

Keating akaribisha tathimini ya sheria ya vyombo vya habari Somalia

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Michael Keating amesema anafahamu kuhusu kuanzishwa kwa sheria ya hivi karibuni katika bunge la Shirikisho la Somalia ambayo litafanyia marekebisho sheria ya vyombo vya habari ya 2016 nchini humo.

Baraza la mawaziri la Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo lilipitisha kifungu cha marekebisho ya sheria ya vyombo vya habari mwezi Julai na kutimiza ahadi aliyoitoa kwa jumuiya za vyombo vya habari wiki chache baada ya kuingia madarakani.

Hata hivyo mabadiliko hayo yalikosolewa na jumuiya za vyombo vya habari na baadhi ya mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu kwa kuanzisha vikwazo vipya katika uhuru wa vyombo vya habari.

Sasa mabadiliko mapya yaliyopendekezwa katika sheria ya vyombo vya habari yatajadiliwa kwenye bunge la shirikisho katika wiki chache zijazo. Umoja wa Mataifa umewataka watunga sheria hao kuyapa uzito malalamiko yaliyowasilishwa na baadhi ya wajumbe wa vyombo vya ahabari vya Somalia kuhusu sheria zilizopo na mapendekezo yaliyopitishwa na baraza la mawaziri la serikali ya shirikisho.

Bwana Keating amesema vyombo vya habari huru na vinavyojitegemea ni muhimu kwa ajili ya uwajibikaji na demokrasia, ambapo baadhi ya sheria za sasa za vyombo vya habari Somalia hazizingatii wiwango vya kimataifa vya sheria za vyombo vya habari.