Saidieni AMISOM ili idhibiti vitisho vya usalama- Balozi Amina

22 Septemba 2017

Kenya imesihi  jumuiya ya kimataifa iongeze zaidi  usaidizi wake kwa ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM ili uweze kushughulikia kwa kina vitisho vya usalama kabla ya kuanza kutekelezwa kwa mpango wa kupunguza idadi ya askari wake.

Ombi hilo limo katika hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Balozi Amina Mohammed wakati akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja waMataifa jijini New York, Marekani siku Ijumaa.

Amesema ili kuimarisha mafanikio yaliyokwishapatikana, Kenya inaunga mkono azimio la Baraza la Usalama lililotathmini majukumu ya msingi ya AMISOM na zaidi ya yote..

(Sauti ya Balozi Amina)

Tunaamini kwamba msaada wa kuwezesha ujenzi mpya wa nchi, ikiwemo kuwezesha serikali kutoa huduma za msingi, kutaongeza imani na kusaidia kuepusha mizozo siku za usoni.”

 

image
Maafisa polisi kutoka Nigeria walioko kwenye ujumbe wa kulinda amani wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM. (Picha:Omar Abdisalan/AMISOM)

Balozi Amina amezungumzia pia mabadiliko ya tabianchi akisema kuwa pamoja na kusababisha mizozo ya rasilimali za maji na ardhi, yanagharimu asilimia 3 ya pato la ndani la taifa kila mwaka.Amesema kwa kutambua hilo..

(Sauti ya Balozi Amina)

“Kenya imepitisha sheria ya kutekeleza mkataba wa Paris. Tumeazimia kupunguza kwa asilimia 30 hewa chafuzi ifikapo mwaka 2030 na badala ya kufanya mambo kwa mazoea, tunatenga fedha pamoja na kusaka teknolojia sahihi na uwezeshaji wananchi kama ilivyokubaliwa Paris.”

Na hatimaye Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Kenya akazungumzia suala la wakimbizi kwa kutambua kuwa Kenya tangu miaka ya 60 imehifadhi wakimbizi kutoka nchi jirani ikiwemo Somalia, hatua ambayo imekuwa na changamoto nyingi ikiwemo za kiusalama.

Amesema ni kwa mantiki hiyo mwaka 2013 Kenya ilitia saini makubaliano ya utatu baina yake, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na serikali ya Somalia kwa lengo la kuwezesha wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiari.

(Sauti ya Balozi Amina)

“Tunatarajia jamii ya kimataifa ituunge mkono katika kuunga mkono mpango huu kwa sababu utawezesha wakimbizi wajenge maisha yao na kurejesha utu wao mbali ya madhila ya kambi za ukimbizi.” 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter