WaYemeni hawana uwezo wa kukomesha vita, ni zaidi ya uwezo wao- McGoldrick

22 Septemba 2017

Hali ya kiusalama nchini Yemen inaendelea kudororo kila uchao wakati mzozo ukiendelea kutokota, mfumo wa afya umesambaratika, uchumi umeporomoka na hali ya kibinadamu inasikitisha.

Kauli hiyo ni kwa mujibu wa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Jamie McGoldrick ambaye ameshiriki mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Yemen uliosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu maswala ya kibinadamu, OCHA leo.

Bwana McGoldrick amesema baada ya takriban miaka miwili ya vita, Yemen inakabiliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu kuwahi kushuhudiwa huku takriban watu milioni 21 wakiwa na mahitaji ya dharura na ulinzi.

Kando na kutoa ombi la ufadhili zaidi, bwana McGoldrick amekumbusha kuhusu umuhimu wa sheria ya kimataifa akisisitiza kuwa cha muhimu ni kumaliza vita. Na kuongeza..

(Sauti ya McGoldrick)

“Tuko hapa kuelezea yanayowasibu waYemen, tumeshuhudia madhila wanayoyapitia na tuko hapa kuwaambia nchi wanachama na wadau na pande husika katika mzozo na wale walio na ushawishi, kuwaambia imetosha! Kwamba madhilia hayapaswi kuwa hali ya kawaida kwa raia Yemen, wameteseka kwa takriban miaka miwili na nusu na hawawezi kukomesha vita, ni zaidi ya uwezo wao. Kwa hiyo ni lazima tufikishe ujumbe huo nyumbani.”