Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Rohingya wakaribia nusu milioni Bangladesh-UNHCR

Wakimbizi wa Rohingya wakaribia nusu milioni Bangladesh-UNHCR

Wakati idadi ya wakimbizi wa Rohingya wanaoingia Bangladesh kutoka Myanmar ikikaribia nusu milioni, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeongeza juhudi za kufikisha msaada wa kuokoa maisha  kwa maelfu ya watu katika kambi mbili za wakimbizi Kusini Mashariki mwa Bangladesh.

Kwa ombi maalumu la serikali ya Bangladesh UNHCR inasema imeharakisha ugawaji wa maturubai ili kuhakikisha watu wengi wanapata ulinzi dhidi ya upepo na mvu za Monsoon, huku wataalamu wake wakisaidia mipango ya ukamilishaji wa makazi mapya ya wakaimbizi katika eneo la Kutupalong la ekari 800 zilizotengwa na serikali ya Bangladesh.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic,  Jumamosi shirika hilo litaanza kugawa vifaa vya jikoni, magodoro, taa za sola na misaada mingine kwa familia 3500 ambazo zimechaguliwa na viongozi wa kijamii.

Ameongeza kuwa wengi wa wakimbizi 420,000 waliowasili Bangladesh wiki tatu zilizopita wamepokelewa na familia katika makambi mawili ya Kutupalong na Nayapara, au wanaishi katika shule na majengo mengine ya umma yaliyogeuzwa makazi ya wakimbizi.

Kamishina Mkuu wa wakimbizi Fillipo Grandi atakuwa Bangladesh Kesho Jumamosi kushuhudia hali halisi, kukutana na wakimbizi na wafanyakazi wa UNHCR.