Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo la tathimini ya haki za binadamu Sudan Kusini lapata mjumbe mpya

Jopo la tathimini ya haki za binadamu Sudan Kusini lapata mjumbe mpya

Rais wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa balozi Joaquín Alexander Maza Martelli wa El Salvador, leo ametangaza uteuzi wa Andrew Clapham wa Uingereza kuwa mjumbe mpya wa jopo lililoundwa na baraza la haki za binadamu kufuatilia na kutathimini hali ya haki za binadamu nchini Sudan Kusini.

Profesa Clapham atajiunga na Yasmin Sooka wa Afrika Kusini, na Godfrey M. Musila wa Kenya ambao uteuzi wao ulitangazwa mwezi juni mwaka 2016.

Profesa Clapham anachukua nafasi ya Kenneth Scott ambaye ameshukuriwa na rais wa baraza balozi Maza Martelli kwa kazi nzuri na huduma aliyoitoa wakati akitekeleza majukumu hayo ya baraza.

Baraza la haki za binadamu liliamua kuanzisha tume ya haki za binadamu nchini Sudan Kusini Machi 2016 kufuatilia na kutoa ripoti kuhusu hali ya haki za binadamu Sudan kusini na pia kufanya mapendekezo kuhusu uwajibikaji.