Ufisadi ni sumu ya maendeleo Haiti :Moise

21 Septemba 2017

Haiti ni kisiwa ambacho kinakabiliwa na changamoto nyingi, kuanzia umasikini, ufisadi, masuala ya afya, majanga ya asili na hata mabadiliko ya taibia nchi.

Lakini kwa kulitambua hilo imejizatiti kuzikabili  kama taifa na kuhakikisha hakuna atakayesalia nyumba.

Hakikisho hilo limetolewa na Rais Jovenel Moise, wa Haiti akihutubia mjadala wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa hii leo New York . Kupitia sauti ya mkalimani Rais huyo amesema ikiwa ni mara yake ya kwanza kuhutubia mjadala huo angependa watu watambue kwamba kama taifa limefungua ukurasa mpya tangu alipoingia madarakani.

(SAUTI YA MOISE 1)

Hakuna shuku kwamba kuanzia mwaka 2017 Haiti imeupa kisogo wakati uliodumaza maendeleo nchini humo, na tangu kuanza kwa Urais wangu mwezi Februari, uongozi wangu umefanya juhudi zote kurejesha demokrasia na utawala wa sheria.

Ameongeza kuwa wanajitahidi kuboresha mfumo wa afya, miundombinu, elimu , tatizo la ajira,  uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na majanga ya asili lakini bado wanakabiliwa na kizingiti kikubwa , ufisadi

(SAUTI YA MOISE2)

"Ufisadi katika mifumo yote unaathiri na kudumaza uchumi, umeutikisa msingi wa kisiasa wa jamii yetu na kuurarua mshikamano wa jamii yetu. Ufisadi ni uhalifu dhidi ya maendeleo, mabilioni ya dola yanatumika na yametumika Haiti na wakati mwingine yanaingizwa katika mikataba ambayo inadhoofisha uchumi wa nchi".

Hivyo amesema sasa umewadia wakati wa misaada yote ya maendeleo kwa Haiti izingatie maslahi ya watu wa taifa hilo na kutouufumbia macho tena ufisadi.