Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kupitia kampeni ya #He4She viongozi 30 wasongesha usawa wa jinsia

Kupitia kampeni ya #He4She viongozi 30 wasongesha usawa wa jinsia

Kando wa mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, viongozi 30 wameweka bayana kile walichofanya kufanikisha usawa wa kijinsia kwenye nchi zao kupitia wakiwa ni mabingwa wa kampeni ya He4She inayotaka wanaume kusimama kidete kutetea haki za wanawake.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UNWomen, Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema hii leo jijini New  York, Marekani wakati huu ambapo matokeo ya kampeni hiyo iliyoanza mwaka 2015 ikidhihirisha mafanikio ikiwemo mabadiliko ya sera na kuweka usawa wa kijinsia.

Mathalani Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema suala muhimu ni kubadilisha fikra za watu na si sheria peke yake na zaidi ya yote kushirikisha waume kama wadau ili kumaliza ukosefu wa usawa.

Naye Rais Arthur Peter Mutharika wa Malawi ambaye nchi yake imafanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa ndoa za umri mdogo kwa wasichana, amesema  kupitia He4She wamepata fursa ya kuwahamasisha wanaume na wavulana juu ya kusongesha haki za wanawake na wasichana.

Kampeni ya He4She imetekelezwa kupitia mpango uitwao IMPACT 10X10X10 ambao kwao viongozi 30, 10 kutoka serikali, 10 kutoka kampuni na 10 kutoka vyuo vikuu wameteuliwa kuwa mabingwa wa kusongesha haki za wanawake na watoto wa kike.