Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto za sasa zinaweza kutatuliwa kupitia teknolojia- Waziri Amina

Changamoto za sasa zinaweza kutatuliwa kupitia teknolojia- Waziri Amina

Ukanda wa Afrika umebeba mzigo mkubwa wa madhara ya misimamo mikali na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha ukame wa muda mrefu na uhaba wa chakula ulioathiri takriban watu milioni 2 na mifugo.

Hiyo ni kauli ya waziri wa Kenya wa mambo ya nje, Amina Mohammed alipohutubia mkutano kuhusu matumizi ya data na teknolojia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kando mwa mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja huo jijini New York, Marekani.

Bi Amina amesema ingawa changamoto zilizokumba nchi nyingi katika ukanda wa Afrika na hususan nchi yake Kenya ni nyingi lakini

“Kenya inaamini kwamba kizazi hiki, kikiwezeshwa kwa  teknolojia mpya na data na ubunifu kitaanza kutatua changamoto za miaka ambazo zimekumba mataifa yetu na watu na kuimarisha ushirikiano wa kweli na unaolenga maslahi halisi ya  watu.”

Aidha waziri Amina ametolea wito kikao hicho kuungana mkono na Kenya na nchi za Afrika kwa ajili ya kuchagiza juhudi za kuwezesha  wakulima wadogo wadogo kutumia data ili kuimarisha uzalishaji.

Halikadhalika kuimarisha ushirikiswaji wa vijana katika biashara ya kilimo na kuboresha ukusanyaji wa data katika wizara kwa kuongeza ufadhili na nguvu kazi.