Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali DRC walindeni wakimbizi:UNHCR

Serikali DRC walindeni wakimbizi:UNHCR

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC imetakiwa kuhakikisha ulinzi kwa raia, wakimbizi na waomba hifadhi baada ya tukio la kushtua na kusikitisha kwenye eneo la Kamanyola nchini humo Septemba 15 ambapo watu 39 walipigwa risasi na kuuawa na wengine 94 kujeruhiwa.

Wito huo umetolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. Limesema tukio la Kamanyola lilitokea baada ya askari wa jeshi la DRC kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji raia wa Burundi Mashariki mwa nchi hiyo ambapo UNHCR inaamini kwamba wengi wao walikuwa ni wakimbizi na waomba hifadhi.

Waliouawa kwenye tukio hilo ni pamoja na wanawake, wanaume na mtoto mmoja, pia askari mmoja wa DRC aliuawa na wengine sita kujeruhiwa.

Kamishina mkuu wa wawakimbizi Filippo Grandi, amesema tukio hilo ni zahma ambayo haikupaswa kutokea, na amekaribisha tangazo la maafisa wa serikali ya DRC lakufanya uchunguzi akiwataka watoe taarifa zake utakapokamilika huku akisisitiza ni lazima kubaini kilichotokea , kuwawajibisha wahusika na kuhakikisha kitendo hicho hakitokei tena.

DRC inahifadhi wakimbizi zaidi ya 43, 700 ambao wamekuwa wakiwasili kutoka Burundi tangu mwaka 2015.