Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu milioni 40 wako utumwani na watoto milioni 152 katika ajira: ILO

Zaidi ya watu milioni 40 wako utumwani na watoto milioni 152 katika ajira: ILO

Utafiti mpya uliofanywa na shirika la kazi duniani kwa ushirikiano na wakifu wa Walk Free, na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM , umebaini kiwango cha utumwa wa kisasa unaoendelea duniani. Flora Nducha na tarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA)

Takwimu zilizotolewa leo wakati wa mjadala wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa  mjini New York Marekani zinaonyesha kwamba zaidi ya watu milioni 40 kote duniani wamekuwa wahanga wa utumwa wa kisasa mwaka 2016.

Pia ILO imetoa takwimu za makadirio ya ajira kwa watoto , zinazothibitisha kwamba takribani watoto milioni 152 wa umri wa kati ya miaka 5 na 17 wako katika ajira ya watoto.

Takwimu hizo zimewataja wanawake na wasichana kuwa ndio waathirika wakubwa wa utumwa wa kisasa wakiwa ni asilimia 71 ya watu wote. Wengi wao wako katika kazi za shuruti, kutumikishwa katika biashara ya ukahaba na asilimia 84 kuingizwa katika ndoa za lazima.

Kwa mujibu wa utafiti huo ajira ya watoto kwa asilimia 70 .9 imesalia katika kilimo, asilimia zaidi ya 17 katika sekta ya huduma na zaidi ya asilimia 11 wakifanyishwa kazi viwandani.

Guy Ryder, mkurugenzi mkuu wa ILO ameonya kwamba dunia haitoweza kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDG’s endapo juhudi zaidi hazitofanyika kukomesha hali hii.