Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Safari ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza NCDs ni ndefu-WHO

Safari ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza NCDs ni ndefu-WHO

Serikali ziimarishe juhudi za kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCDs ili kufikia malengo yaliyowekwa ikiwemo kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika, imesema ripoti mpya ya shirika la afya ulimwenguni, WHO iliyotolewa leo.

WHO imesema ni hatua kidogo tu zimepigwa ikiwemo katika magonjwa ya moyo, magonjwa sugu ya kupumua, saratani na kisukari ambayo yanasababisha vifo vingi zaidi na kuua takriban watu milioni 15 duniani walio na umri kati ya miaka 30-70.

Vipimo vya WHO kwa mwaka 2017 vinavyochagiza nchi kuweka malengo, na sera kukabiliana na hatari za NCDs ikiwemo matumizi ya tumbaku, lishe duni, ukosefu wa mazoezi na matumizi ya vileo kupindukia pamoja na kuboresha uwezo wa kutibu NCDs,  vinaonyesha kwamba hatua kote ulimwenguni ni finyu na sio sawa.

Aidha asilimia 80 ya vifo vinatokea katika nchi zinazoendelea ambako gharama kutokana na magonjwa ya NCDs inakadiriwa kuwa dola trilioni 7.

Dkt. Douglas Bettcher ni kutoka idara ya kinga ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza WHO

“Fursa ya kuokoa maisha inadidimia, na hili linafanyika mbele ya macho yetu kwa njia nyingi ikiwemo kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu- hususan watoto na barubaru ambao wana utipwautipwa na kisukari. Iwapo hatutachukua hatua sasa na kulinda watu dhidi ya NCDs, tutasababisha vijana wa leo na kesho kuishi maisha yenye fursa chache za kiuchumi.”

Dkt. Bettcher amesema ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ni lazima kupunguza kwa theluthi moja idadi ya vifo vinavyosabibishwa na NCDs.