Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM utajikita na vitendo zaidi ili kupunguza gharama na kuzaa matunda: Guterres

UM utajikita na vitendo zaidi ili kupunguza gharama na kuzaa matunda: Guterres

Umoja wa Mataifa umejizatiti kuhakikisha kwamba unafanya marekebisho yanayohitajika ikiwemo kuepuka ukiritimba na kuzingatia misingi ya katiba ya Umoja huo.  Flora Nducha na tarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA)

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika mkutano maalumu wa ngazi ya juu kuhusu marekebisho ya Umoja wa Mataifa uliofanyika leo hapa New York Marekani.

Mkutano huo ambao umeongozwa na Rais wa Marekani Donald J Trump na Katibu Mkuu umejikita katika kuhakikisha fedha zinazotolewa na nchi wanachama zinaenda sanjari na matakwa ya dunia na misingi ya katiba ya Umoja wa Mataifa, lakini pia kubana matumizi. Akiutaka Umoja wa Mataifa kuzingatia hayo Rais Trump amesema...

image
Rais wa Marekani Donald J Trump akihutubia mkutano maalumu wa ngazi ya juu kuhusu marekebisho ya Umoja wa Mataifa. Picha: UM/Idhaa ya Kiswahili
(Sauti ya Trump)

“Umoja wa Mataifa haujafikia kilele cha utendaji wake kwa sababu ya urasimu na kutowajibika ipasavyo , bajeti yake imeongezeka na wafanyakazi wake wameongezeka zaidi ya mara mbili tangu mwaka 2000, hatujaona matokeo yanayoenda sanjari na uwekezeji wetu na tunatoa wito wa Umoja wa Mataifa kujikita zaidi na watu

Naye Katibu Mkuu Guterres akihakikisha mwito huo utatekelezwa amesema

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres(kushoto) na Rais wa Marekani Donald J. Trump. Picha: UM/Idhaa ya Kiswahili
(Sauti ya Guterres)

“Kwa pamoja tunapiga hatua katika kuleta mabadiliko kwenye Umoja wa Mataifa na kuuimarisha , tumezindua mkakati wa kumaliza unyanyasaji na ukatili wa kingono , kuleta usawa wa kijinsia , kuwalinda wafichua tarifa na kukabili ugaidi, na tunafanyia mabadiliko mfumo wetu wa operesheni za ulinzi wa amani ili kuuimarisha na kuhakikisha unakuwa wa gharama nafuu.”

Pia amesisitiza urasimu utapatiwa dawa mujarabu na kuhakikisha fedha zinazotolewa na nchi wanachama zinafanya kazi iliyokusudiwa.

Rasimu ya marekebisho hayo iliwasilishwa na Marekani ambapo hadi sasa nchi 122 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa wameridhia na miongoni mwao ni Rwanda.