Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 150,000 wa Rohingya kuchanjwa dhidi ya surua, polio na Rubella:

Watoto 150,000 wa Rohingya kuchanjwa dhidi ya surua, polio na Rubella:

Kampeni ya chanjo dhidi ya surua, rubella na polio imeanza kwa lengo la kuwachanja watoto wakimbizi Rohingya 150,000 nchini Bangladesh walio chini ya umri wa miaka 15 katika makazi 68 ya wakimbizi karibu na mpaka na Myanmar.

Kampeni hiyo ya siku saba inaongozwa na wizara ya afya kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEFna shirika la afya duniani WHO.

UNICEF inaisaidia wizara ya afya kwa kutoa dawa za chanjo, mabomba ya sindano na tembe za vitamin A. Huku WHO kwa upande wake imeandaa kampeni nzima ya chanjo na inasimamia na kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha kila mtoto anafikiwa.

Zaidi ya wakimbizi 410,000 wa Rohingya wamewasili Bangladesh tangu Agosti 25 na maelfu wengine wanaendelea kuwasili kila siku. Kwa mujibu wa makadirio ya awali watoto ni asilimia 60 ya wakimbizi hao.