Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi ya 370,000 wahitaji matibabu ya utapia mlo Kenya-UNICEF

Watoto zaidi ya 370,000 wahitaji matibabu ya utapia mlo Kenya-UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema, takriban watoto 370,000 wanahitaji matibabu dhidi ya utapiamlo uliokithiri nchini Kenya kufuatia kiangazi cha muda mrefu kwa sababu ya mvua chache  kati ya Machi na Juni, ikiwa ni msimu wa tatu wa mvua chache tangu mwaka 2016.

Shirika hilo limeongeza kuwa mwaka huu watoto wengine 37,000 wametumbukia kwenye utapiamlo huku 72,600 wakiwa na unyafuzi na kuhitaji huduma ya haraka ya kuokoa maisha.

Kwa mujibu wa Werner Schultink, mwakilishi wa UNICEF Kenya hadi sasa wamewafikia watoto asilimia 60 kwa msaada wa kuokoa maisha mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana. Amesema ili kupunguza adha hiyo kunahitajika fursa kubwa ya kuwafikishia watoto lishe bora, maji safi na huduma za afya ili walio katika hatari waweze kunusurika.

Amesema katika tafiti nne kati ya 17 walizozifanya kati ya Juni na Julai mwaka huu nchini Kenya utapiamlo umeongezeka mara mbili ya kiwango cha hatari cha asilimia 15.