Suluhu na matokeo yanayoonekana vyahitajika kwa ajili ya watu: Lajčák

Suluhu na matokeo yanayoonekana vyahitajika kwa ajili ya watu: Lajčák

Rais mpya wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 72, amesema anatarajia kutoa ufumbuzi halisi na matokeo kwa watu wakati wa muhula wake wa kusimamia kazi za wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa.

Miroslav Lajčák, mwanadiplomasia mkongwe kutoka Slovakia Ulaya Mashariki  akizungumza na UN News kabla ya kuanza rasmi jukumu la kuongoza kikao cha 72 cha baraza kuu leo , ametaja masuala atakayoyapa kipaumbele na kuweka matumaini yake.

(Sauti ya Lajčák)

“Kwanza ni kuzuia migogoro , tunazungukwa na mizozo mingi na suluhu kiduchu, hivyo natajajia kutoa msukumo wa nini tukifanye vyema ili kuepuka migogoro, na matumaini yangu ya pili ni suala linalohusiana na uhamiaji, ni suala la kimataifa , ni suala linalotukabili sote na tuna kazi  na tuna wajibu wa kuandaa muongozo wa kimataifa wa uhamiaji , ni suala litakalochukua nafasi kubwa ya kikao cha 72, lakini ni matumaini yangu kwamba tutaweza kuwasilisha nyaraka ya kuaminika itakayopokewa na raia wetu.”

Pia ameahidi muhula wake utakuwa ni mwaka wa kujaribu kupata muafaka wa masuala kadhaa miongoni mwa nchi wanachama na kujaribu kuboresha maisha ya watu duniani.

image
Miroslav Lajčák (katikati), Rais wa kikao cha 72 cha Baraza Kuu la UM akigonga nyundo kuashiria kuanza kwa kikao. Kushoto ni Katibu Mkuu António Guterres na kulia ni Catherine Pollard, Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya mikutano. (Picha: UN /Kim Haughton)
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha 72 cha baraza kuu amesema dunia hivi sasa imeghubikwa na changamoto nyingi kuanzia masuala ya silaha za nyuklia, ugaidi, mabadiliko ya tabia nchi vita hadi uhamiaji na mkakati anaoingia nao bwana Lajcak wa kujikita na watu unaleta matumaini huku akiahidi kushirikiana naye.

 (Sauti ya Guterres)

"Watu kote duniani wanadai mabadiliko na wanaziangalia serikali na taasisi kutimiza hilo, wote tunaafiki kwamba Umoja wa Mataifa unahitaji kujitahidi zaidi kubadilika na kutimiza ahadi, na hilo ndio lengo la mapendekezo ambayo yatajadiliwa na hili baraza kuu na ninatarajia kufanyakazi pamoja nawe mheshimiwa Rais na wawakilishi wa kudumu ili kuimarisha shirika letu na ili kuwasaidia vyema nchi wanachama na kutoa matokeo mazuri kwa watu tunaowahudumia.”