Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 50 ya ukaliwaji Palestina imeleta umasikini na kudumaza maendeleo:UNCTAD

Miaka 50 ya ukaliwaji Palestina imeleta umasikini na kudumaza maendeleo:UNCTAD

Mwaka huu inatimia miaka 50 tangu Israel ianze kulikalia eneo la Wapalestina huko Ukanda wa Gaza na ukingo wa Magaribi ikiwa ni pamoja na eneo la Jerusalem Mashariki .

Ukaliwaji huu ni wa muda mrefu zaidi katika historia ya karibuni na kwa Wapalestina ni miongo mitano iliyoghubikwa na kutokuwa na maendeleo, kukandamizwa kwa watu na kunyimwa haki za maendeleo.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo UNCTAD, iitwayo msaada wa mendeleo wa UNCTAD kwa watu wa Palestina.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba ukaliwaji wa eneo la Wapalestina umeiua sekta ya kilimo na viwanda na kudhoofisha uwezo wa uchumi wa eneo hilo kuweza kushindana nyumbani na nje ya eneo hilo.

Ripoti imeongeza kwamba pato la taifa (GDP) katika eneo linalokaliwa la Wapalestina bado lipo kwenye kiwango kilekile kilichokuwa mwaka 1999, na hili ni dhihirisho la gharama wanaozibeba raia wa Palestina na kupotea kwa fursa za kiuchumi kutokana na kukaliwa huko.

Ripoti ya UNCTAD imeongeza kuwa hali imezidi kuwa mbaya kutokana na vikwazo vya Isarel katika kuingiza na kusafirisha bidhaa , kubinya uwekezaji, umasikini  na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira hali ambayo ripoti inasema itaendelea katika kipindi kilichosalia cha mwaka huu wa 2017.