Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shehena ya usaidizi kwa warohingya yawasili Bangladesh

Shehena ya usaidizi kwa warohingya yawasili Bangladesh

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limefikisha shehena ya kwanza ya misaada ya dharura kwa warohingya wa Myanmar waliosaka hifadhi nchini Bangladesh.

Ndege mbili zilizosheheni zaidi ya tani 91 za misaada hiyo ikiwemo vifaa vya malazi zimewasili mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka, moja ikiwa imekodishwa na UNHCR ilhali nyingine imekodishwa na falme za kiarabu.

UNHCR inasema hivi sasa warohingya zaidi ya 370,000 wasio na utaifa wamekimbilia Bangladesh kutoka Myanmar tangu tarehe 25 mwezi uliopita na idadi inatarajiwa kuongezeka.

Wakati huo huo, kamishna msaidizi wa UNHCR anayehusika na operesheni George Okoth-Obbo yuko eneo la Cox Bazar ambako misaada hiyo inapelekwa na baadaye atakutana na familia hizo za warohingya na mamlaka za Bangladesh.