Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji wanakabiliwa na hatari kubwa ya kutoweshwa: UM

Wahamiaji wanakabiliwa na hatari kubwa ya kutoweshwa: UM

Kuna uhusiano kati  ya watu kutoweshwa na uhamiaji, lakini serikali na jumuiya ya kimataifa hawatilii maanani suala hili, limeonya leo kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa katika ripoti yao mpya waliyoiwasilisha kwenye baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi.

Kikosi kazi kinachohusika na watu kutoweshwa kwa lazima au pasi ridhaa yao kimesema kutoweshwa kwa wahamiaji ni suala mtambuka linalohitaji kutambulika na kushughulikiwa kimataifa.

Kundi hilo limesema kwa ujumla nchi na jumuiya ya kimataifa hawajaweka mtazamo thabiti katika suala hili, asili yake na mapana yake, wanalifumbia macho, na kusukuma lawama kwingineko , kwa nchi nyingine au kwa magenge ya uhalifu.

Ripoti yao inabainisha kwamba baadhji ya watu wanahama kwa sababu ya vitisho au hatari ya kutoweshwa nchini mwao au kutoweka wakiwa safarini, au kwenye nchi walikokwenda.

Wameongeza kuwa hii inatokea kwa sababu ya utekaji wa kisiasa au sababu zingine katika minajili ya watu kuwekwa rumande, katika mchakato wa kuruidishwa walikotoka, au kama athari za usafirishaji haramu wa binadamu.

Wataalamu hao wamesisitiza ni muhimu kwa kila nchi kulichukulia tatizo hili kwa uzito na kuimarisha hatua za haraka za kuzuia na kukabiliana nalo katika ngazi ya kitaifa, lakini pia kuimarisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa katika ngazi ya kikanda na kimataifa.