Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya inahitaji dola 106M kufuatia ukame unaokumba eneo la Kaskazini mwa nchi

Kenya inahitaji dola 106M kufuatia ukame unaokumba eneo la Kaskazini mwa nchi

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yametoa ombi la dola milioni 106 kwa ajili ya kupiga jeki shughuli za za dharura za kuokoa maisha kufuatia ukame unaokumba eneo la Kaskazini mwa Kenya.

Akizungumza wakati wa kutoa ombi hilo Siddharth Chatterjee, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya amesema jamii ya Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa inashikamana na serikali na watu wa Kenya kwa ajili ya kukabiliana na athari za ukame katika jamii zilizoko kwenye hatari zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani Stéphane Dujarric msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema

(Sauti ya Dujarric)

“Ombi la awali lilitolewa mnamo Machi mwaka huu lakini ni asilimia 43 tu ya ombi hilo limefadhiliwa huku janga la ukosefu wa chakula na utapiamlo likishamiri kwa ajili ya ukame wa mara kwa mara. Takribani watu milioni 5.6 wameathirika na ukame huo ikiwemo watu milioni 3.4 ambao hawana uhakika wa chakula huku takriban watoto laki tatu wanaoishi katika maeneo kavu wakihitaji tiba dhidi ya utapiamlo.”

Ombi jipya lililotolewa ni kwa ajili ya mwezi wa Septemba hadi Desemba mwaka huu kuendana na mpango wa serikali.

Tangu Novemba 2016 serikali ya Kenya imetenga dola milioni 124.3 kwa mpango wa awamu ya kwanza na ya pili lakini awamu ya tatu huenda ikachelewa kufuatia hali ya kisiasa inayoshuhudiwa na hivyo amesema ni muhimu wafadhili waitikie wito wa ombi hilo.