Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupindu chaua watu 23 Nigeria

Kipindupindu chaua watu 23 Nigeria

Mlipuko wa kipindupindu umeripotiwa katika jimbo la Borno nchini Nigeria ambapo wizara ya afya nchini humo imesema hadi sasa watu 23 wamefariki dunia tangu kisa cha kwanza kiripotiwe tarehe 16 mwezi uliopita.

Idadi hiyo ya vifo ni kati ya wagonjwa 530 walioripotiwa hadi jana kwenye kambi ya Muna Garage inayohifadhiwa wakimbizi wa ndani 20,000 katika vitongoji vya mji Maiduguri jimboni Borno.

Ripoti zinasema kuwa licha ya kwamba visa vingi vimeripotiwa katika kambi ya Muna Garage, vingine vimeripotiwa katika kambi ya Custom House, Ruwan Zafi na Bolori II huku visa vingine vikishukiwa katika maeneo ya Monguni na Dikwa.

Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na wizara ya afya na mashirika ya kibinadamu wanahaha kukabiliana na mlipuko huo ambako kituo cha shughuli za dharura kimeanzishwa kwa ajili ya kukabiliana na hali ya sasa.

Aidha kituo hicho kinachagiza usafi huku wanaoshukiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa kipundupindu wakishauriwa kupimwa.