Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya Kipindupindu zapelekwa Sierra Leone

Chanjo dhidi ya Kipindupindu zapelekwa Sierra Leone

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema nusu ya wananchi wa Sierra Leone watapatiwa chanjo dhidi ya Kipindupindu ili kuwakinga na ugonjwa huo baada ya mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyokumba nchi hiyo mwezi uliopita.

WHO imenukuu wizara ya afya nchini humo ikisema kuwa hatua hiyo inafuatia mfuko wa chanjo duniani, GAVI kupeleka zaidi ya chanjo milioni moja na walengwa zaidi ni wakazi wa maeneo yaliyokumbwa zaidi kwenye mji wa Regent na viunga ya mji mkuu Freetown.

Dozi itatolewa kwa kila mtu mara mbili ambapo afisa mtendaji mkuu wa GAVI Dkt. Seth Berkley amesema upelekaji wa chanjo hizo utazuia mlipuko wa Kipindupindu wakati huu ambapo huduma za maji safi na kujisafi bado zinakabiliwa na changamoto.

Zaidi ya watu 500 walifariki dunia kwenye zahma hiyo huku mamia zaidi bado hawajulikani walipo na maelfu wamepoteza makazi yao.