Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Diplomasia ya hali ya juu yahitajika dhidi ya DPRK- Feltman

Diplomasia ya hali ya juu yahitajika dhidi ya DPRK- Feltman

Kwa mara nyingine tena Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana leo kujadili kitendo cha Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK kufanya jaribio la kombora na wakati huu likiwa ni kombora la nyuklia, jaribio lililofanyika chini ya ardhi jana Jumapili.

Mkuu wa masuala ya siasa kwenye umoja huo, Jeffrey Feltman amewaambia wajumbe kuwa kitendo hicho kinazidi kutia wasiwasi hasa wakati huu ambapo imeelezwa DPRK inajipanga kufanya jaribio la kombora lingine la masafa marefu licha wito wa kutakiwa kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Bwana Feltman amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anategemea Baraza la Usalama liendelee kuungana na kuchukua hatua sahihi kwa kuwa kadri mvutano unavyoongezeka, vivyo hivyo kutokuelewana na kuchukua hatua zisizo sahihi.

Kwa mantiki hiyo amesema..

 (Sauti ya Feltman)

“Matukio makubwa ya hivi karibuni yanahitaji hatua za kina ili kuondoa mwendelezo wa vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na DPRK. Hatua hizo ili ziwe na ufanisi lazima ziwe za busara na diplomasia ya hali ya juu.”

image
Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye UM Balozi Nikki Haley, akihutubia Baraza. (Picha:UNWebtv video)
Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Nikki Hailey ambaye ni mmoja wa wajumbe walioomba kuitishwa kwa kikao cha leo, amesema maazimio lukuki yaliyopitishwa na Baraza hilo hayajaleta mabadiliko yoyote na sasa DPRK inapanga mikakati mipya. Kwa mantiki hiyo amesema..

(Sauti ya Balozi Nikki)

“Wamiliki wa nyuklia wanatambua wajibu wao. Yaonekana Kim Jong-Un hatambui. Matumizi yake mabaya ya makombora na vitisho vya nyuklia yaonekana anaomba vita. Vita si kitu ambacho Marekani inataka. Hatuhitaji sasa.”

Japan nayo ilipata fursa kuwasilisha hoja yake kupitia mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Koro Bessho ambaye naye amesema nchi yake imeguswa sana na hatua za umoja huo na mataifa mengine kulaani kitendo cha DPRK lakini ..

(Sauti ya Balozi Bessho)

“Lakini zaidi ya kulaani, Baraza la Usalama lazima lichukue hatua kuzuia Korea Kaskazini kuendelea na mwelekeo huu. Ni lazima tuweke bayana kwa Korea Kaskazini kuwa mwendelezo wa sera ya sasa unaweza kuleta athari mbaya sana.”