Mamlaka Myanmar ina wajibu katika kuzuia janga-Guterres

Mamlaka Myanmar ina wajibu katika kuzuia janga-Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea kusikitishwa sana na ripoti za operesheni katili za kiusalama zinazotekelezwa dhidi ya raia katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar, wakati huu ambapo maelfu ya watu wa kabila la Rohingya wakikimbilia nchi jirani ya Bangladesh.

Kupitia taarifa ya msemaji wake Guterres amesema watu wanahitaji kujizuia ili kuepukana kutokea kwa janga la kibinadamu huku akitolea wito utulivu na kukumbusha kwamba serikali ina wajibu wa kuhakikisha usalama na msaada kwa wale wenye mahitaji na kuruhusu Umoja wa Mataifa na wadau kufikisha msaada.

Halikadhalika Katibu Mkuu amesema wimbi la vurugu zilizoanza wiki jana na mashambulizi ya vikundi vya waasi dhidi ya serikali vinahitaji kukabiliwa kiujumla ili kutatua mizizi inayochochea vurugu.

Guterres ameshukuru juhudi za mamlaka Bangladesh na jamii ambao wanajaribu kutimiza mahitaji muhimu ya wakimbizi wanaokimbilia usalama.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba zaidi ya warohingya 27,000 wengi wao wakiwa waislamu wamekimbia nchi jirani huku maelfu wakiripotiwa kukwama.