Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna uhusiano kati ya dhoruba Harvey na shughuli za binadamu- WMO

Kuna uhusiano kati ya dhoruba Harvey na shughuli za binadamu- WMO

Jopo la wataalamu kutoka shirika la hali ya hewa duniani, WMO limesema kuna uwezekano mkubwa kuwa athari za binadamu kwenye tabianchi zimesababisha dhoruba Harvey iliyopiga jimbo la Marekani la Texas.

Katika taarifa yao, jopo hilo la wataalamu saba limesema uhusiano huo unaweza usiwe wa moja kwa moja lakini wamezingatia suala kwamba mvua kubwa iliyoambatana na dhoruba hiyo imekuwa mbaya zaidi kutokana na shughuli za binadamu.

Mathalani wametaja harakati za kuendeleza maeneo ya fukwe zimesababisha uharibifu mkubwa wa maeneo ya pwani za Marekani.

Wamesema shughuli hizo pia zinasababisha kuongezeka kwa kiwango cha unyevunyevu kwenye anga na kuleta mvua na kwamba dhoruba inayotokea katika maeneo yenye joto ina uwezo wa kuleta hatari kubwa zaidi.

Kwa mantiki hiyo wameonya kuwepo wa uwezekano wa dhoruba zaidi katika karne hii ya 21 kutokana na kiwango cha joto ulimwenguni kuongezeka.

Hadi sasa yaripotiwa kuwa watu 47 yaripotiwa wamefariki dunia kutokana na dhoruba Harvey huko Texas, maelfu wamepoteza makazi huku mamlaka zikiendelea kutafuta watu ambao hawajulikani walipo.