UNIFIL yaongezewa mwaka mmoja, Guterres apongeza

1 Septemba 2017

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kupitisha kwa kauli moja azimio linaoongeza muda wa ujumbe wa umoja huo nchini Lebanon, UNIFIL hadi tarehe 31 Agosti 2018.

Muda wa ujumbe huo ulikuwa  umalizike leo na sasa kufuatia kuongezwa muda, Katibu Mkuu amesema UNIFIL kwa kushirikiana kwa karibu na jeshi la Lebanon wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa azimio hilo namba 2373.

Kwa mantiki hiyo kupitia taarifa ya msemaji wake, amesihi jamii ya kimataifa iendelee kusaidia serikali ya Lebanon kwa minajili hiyo ili kuepusha mizozano kwenye eneo la kusini mwa nchi hiyo kati yake na Israel.

Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa pande husika kutumia utulivu uliopo na kujikita kwenye lengo la kuwa na sitisho la kudumu la mapigano na hatimaye kushughulikia masuala yaliyosalia kwa mujibu wa maazimio tangulizi kama lile namba 1701.

Ametumia fursa hiyo pia Katibu Mkuu kushukuru mataifa ambayo yanachangia askari kwenye ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL.

UNIFIL ilianzishwa tarehe 19 Machi mwaka 1978 kufuatia mzozano kusini mwa Lebanon kati yake na Israel ikidaiwa kuwa wapiganaji wa Hezbollah wanahusika na ghasia hali iliyosababisha Israel kusogeza vikosi vyake.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter