Vita vya kunyakua Raqqa havipaswi kugharimu raia-Zeid

31 Agosti 2017
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa , Zeid Ra’ad Al Hussein, amesisitiza kwamba vita vya kunyakua Al-Raqqa na Deir-ez-Zor kutoka kwa kundi la ISIL havipaswi kugharimu maisha ya raia walioko katika maeneo yaliyozingirwa.

Zeid ameongeza kwamba lengo la kushindwa kwa ISIL ni kulinda na kusaidia raia ambao wameteseka kupitia mfumo wa kundi hilo wakati huu ambapo kumeripotiwa idadi kubwa ya majeruhi na kuendelea kwa mashambulizi ya anga Raqqa na matumizi ya raia kama ngao vitani.

Kamishna mkuu ameelezea wasiwasi wake kuhusu  raia wasio na hatia kuendelea kulipa gharama kubwa ya vita, wakati ambapo raia 20,000 wamekwama mji wa Al-Raqqa na wengine katika mji wa Deir-ez-Zor ikiwemo watoto.

Halikadhalika ametolea wito pande husika kuheshimu wajibu wao katika sheria ya kibinadamu na sheria ya kimataifa kulinda raia na mali zao. Aidha ametaka wanaokiuka sheria za kimataifa kuchunguzwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter