Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasyria wasilipe gharama ya mkwamo wa kisiasa- O’Brien

Wasyria wasilipe gharama ya mkwamo wa kisiasa- O’Brien

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura akihutubia kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi (Picha:UN/Kim Haughton)Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limeshauriwa kusaka njia ya kuondokana na mwelekeo wa sasa huko Syria ambako raia wasio na hatia wanalipa gharama ya mkwamo wa mchakato wa kisiasa.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa kibinadamu, OCHA, Stephen O’Brien amesema hayo leo alipohutubia Baraza la Usalama jijini New  York, Marekani, ikiwa ni mkutano wake wa mwisho wakati huu ambapo anahitimisha jukumu hilo.

Bwana O’Brien amesihi chombo hicho cha wanachama 15 kuchukua hatua zaidi ili kumaliza vita nchini Syria vilivyodumu kwa miaka saba sasa…

(Sauti ya O’Brien)

"Nawasihi ninyi, kwa msingi wa ubinadamu msake njia ya kusitisha gharama ambayo wananchi wa Syria wanalipa kutokana na mkwamo wa kisiasa. Suala kwamba mwezi baada ya mwezi, hali inaendelea kuwa mbaya, machungu wanayopata wananchi wa Syria yanachoma nyoyo zetu na kujikita kwenye fikra zetu. Kwa kweli tunaweza kuchukua hatua zaidi.”

image
Mtoto asimama karibu na jengo lilioporomoka. Picha: UNICEF
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura akihutubia kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi amesema ghasia zinaendelea kupungua nchini humo lakini suala nyeti zaidi ni kupata njia salama na uhakika za kufikisha misaada ya kibinadamu.

Bwana de Mistura ametoa wito kwa pande zote za mzozo wa Syria kuwa na dira moja kuelekea utekelezaji wa mazungumzo ya amani yanayofanyika Geneva ambayo yanaratibiwa na Umoja wa Mataifa.