Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji 50 wa Ethiopia waliokwama puntland warejea nyumbani- IOM

Wahamiaji 50 wa Ethiopia waliokwama puntland warejea nyumbani- IOM

Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM, limewezesha wahamiaji 50 wa Ethiopia waliokuwa wamekwama kwenye eneo lililojitenga la Puntland huko Somaliland kurejea nyumbani.

Miongoni mwao ni wanaume 29 , wanawake 5 na watoto 16 na walirejea nyumbani kwa hiari kwa ushirikiano baina ya wizara ya mambo ya  ndani ya Puntland , kituo cha dharura cha uhamiaji Bossaso, chama cha Jumuiya ya Ethiopia nchini Bossaso pamoja na  ofisi ya ubalozi ya Ethiopia  ambapo mpango ulifadhiliwa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Haille, ambaye ni mmoja wa wahamiaji hao amesema walikwama Bossaso huko Puntland kwa miaka mitano yeye pamoja na mkewe na watoto wanne, na kwamba mkewe alienda Mashariki ya Kati miezi michache iliyopita kutafuta kazi.

Hivi sasa Haille amesema maisha yamekuwa magumu kwa kuwa hawezi kulea watoto peke yake na hivyo ameamua kurejea nyumbani Ethiopia.

IOM inasema wahamiaji wanaosafirishwa kupitia Bossaso, Puntland, wanakabiliwa na hatari kadhaa ikiwa ni pamoja na kutekwa nyara na aina nyingine za  unyanyasaji.