Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo endelevu na amani haviwezi kuachana- Amina

Maendeleo endelevu na amani haviwezi kuachana- Amina

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha kuangazia mchango wa operesheni za ulinzi wa amani za umoja huo katika kuchagiza jitihada za kudumisha amani duniani.

Akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesema ni dhahiri shahiri kuwa ajenda ya maendeleo endelevu iliyopitishwa haiwezi kufanikiwa iwapo hakuna amani.

Halikadhalika bila amani maendeleo endelevu yatasalia kuwa ni ndoto na kwamba vyote viwili haviwezekani bila uzingatiaji wa haki za binadamu.

(Sauti ya Amina)

“Kufanikisha amani na maendeleo endelevu, tunahitaji kushiriki kwa pamoja katika hatua na kuchagiza ushirikiano na udau, ikiwemo wafanyabiashara, taasisi za fedha, mashirika ya kiraia na taasisi za kikanda.”

image
Polisi wanawake walio katika kikosi cha pamoja cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, huko Darfur nchini Sudan, UNAMID. (Picha:UN/Albert González Farran)
Bi. Amina akaenda mbali zaidi kuangazia mchango wa wanawake katika ulinzi wa amani akisema uwepo wao umedhihirisha uwezo wao sawa na wanaume na hivyo..

(Sauti ya Amina)

“Ni jambo muhimu kuajiri walinda amani na polisi wanawake na kuendelea kuwa nao siyo tu kwa sababu kuziba pengo la kijinsia, bali pia kwa sababu uwepo wa wanawake umeongeza fursa za kudumisha amani na kupunguza visa vya ukatili wa kingono.”

Kwa mantiki hiyo Naibu Katibu Mkuu amesihi Baraza la Usalama lielekeze juhudi na rasilimali katika kufanikisha lengo la kuwa na amani endelevu na kudumisha amani.