Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani jaribio la kombora kutoka DPRK

Guterres alaani jaribio la kombora kutoka DPRK

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amelaani jaribio la hivi karibuni zaidi la kombora la masafa marefu lililofanywa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa jaribio la kombora hilo lilifanyika jana na lilivuka kisiwa cha Japan.

Kufuatia taarifa hizo, Bwana Guterres amesema kitendo hicho ni kinyume na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia kinatishia usalama na utulivu wa kikanda, sambamba na kufifisha jitihada za mazungumzo.

Katibu Mkuu ameitaka DPRK kuzingatia wajibu wake kimataifa na kufungua milango ili mazungumzo kuhusu suala hilo yaweze kufanyika huku akisema anaendelea kuwasiliana na pande zote husika kwenye jambo hilo.

Katika hatua nyingine Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baadaye leo litakuwa na kikao kuhusu sakata hilo la DPRK na majaribio ya makombora.