Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu ana wajibu wa kutatua changamoto ya maji- Thompson

Kila mtu ana wajibu wa kutatua changamoto ya maji- Thompson

Wakati kongamano la kuadhimisha wiki ya maji duniani likiwa limeingia siku ya pili huko mjini Stockholm, Sweden rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Peter Thompson amesema suala la maji na huduma za kujisafi ni muhimu katika malengo 17 ya maendeleo endelevu  yaani SDGs.

Maudhui ya wiki ya maji mwaka huu ni “Maji na taka: Punguza na tumia tena” ambapo Bwana Thompson amesema, wakati hatua za miongo kadhaa zimetekelezwa, ni sahihi kufikiria kwamba changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama na huduma za kujisafi ni suala ambalo lingekuwa limeshatatuliwa lakini…

(Sauti ya Thompson)

“Cha kusikitisha ni kwamba hilo sio sahihi. Takriban watu bilioni 2.4 hawana huduma za kujisafi. Na idadi kubwa ya wati kwenye kanda na  nchi wanakabiliana na uhaba wa maji unaochagizwa na kuongezeka kwa idadi ya watu, kukua kwa miji na pia mabadiliko ya tabianchi.”

Aidha ametolea wito kila mtu kuwekeza katika juhudi za pamoja katika kufikia lengo namba sita la SDGs kuhusu maji na huduma za kujisafi akiongeza..

(Sauti ya Thompson)

“Ninapongeza kongamano hili la wiki ya maji kwa kutuleta pamoja kujadili changamoto za kizazi chetu na kufahamu tulivyounganishwa. Kaskazini na Kusini, Mashariki na Magharibi, bahari inatuunganisha sote na ni lazima tulete utu katika mahusiano ili kuwa na usawa na heshima kati yetu na maji.”

Mkutano huo ulioanza jana utahitimishwa Septemba Mosi ambapo wa wadau mbalimbali wanashiriki wakiwemo, wataalam, watunga sera, wafanyabiashara wabunifu na vijana kutoka nchi mbali mbali kwa ajili ya kubonga bongo kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto zinazoendana na upatikanaji wa maji.