Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi Yemen waendelea kudhibiti Kipindupindu licha ya kukosa mishahara

Wafanyakazi Yemen waendelea kudhibiti Kipindupindu licha ya kukosa mishahara

Shirika la kuhudumia watoto duniani UNICEF leo katika ripoti yake limesema kasi ya kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini Yemen imepungua.

Limesema hali hiyo inatokana na juhudi za wananchi kwa msaada wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine kupiga vita ugonjwa huo hatari.

Naibu mkurugenzi wa kitengo cha kipindupindu katika hopitali Alsadaqah jijini Aden Dkt.  Nahla Arishi amesema wamekuwa na wakati mgumu kuwahudumia wagonjwa kwa kuwa zahanati imezidiwa uwezo.

Hata hivyo ameseam yeye mwenyewe akiwa ni mzazi hawezi kufungia milango wagonjwa kwa kuwa wahitaji  ni wengi.

UNICEF inasema wafanyakazi wa afya, na wale wanaohusika na maji safi pamoja na mazingira hawajapokea mishahara yao kwa miezi 10 sasa lakini wamekuwa mstari wa mbele kujitolea kupambana na mlipuko huo wa kipindupindu, mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.

Hadi sasa watu Laki tano na nusu wamekadiririwa kuathiriwa na ugonjwa huo huku wengine 2000 wakifariki dunia na nusu yao ni watoto.

Kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa kipindupidnu bado inaendelea Yemen ambapo inakadiriwa kuwa watu milioni 12 wamefikiwa na kampeni hiyo inayoendeshwa na wafanyakazi elfu 40 wa kujitolea.