Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP inahitaji fedha zaidi kwa ajili ya wakimbizi walioko Tanzania

WFP inahitaji fedha zaidi kwa ajili ya wakimbizi walioko Tanzania

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limelazimika kupunguza mgao wa chakula kinachotolewa kwa wakimbizi 320,000 wanaoishi katika kambi za Mtendeli, Nduta na Nyarugusu mkoani Kigoma kaskazini magharibi mwa Tanzania kwa sababu ya upungufu wa fedha.

WFP inahitaji kwa haraka jumla ya Dola za Marekani milioni 23.6 kuanzia sasa hadi Desemba, 2017 ili imudu kuendelea kutoa mgao unaokidhi mahitaji ya chakula na lishe kwa wakimbizi wanaoishi nchini Tanzania.

WFP hutoa msaada wa chakula mbali mbali kwa wakimbizi kambini kutoka  Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Vyakula hivi ni pamoja na unga wa mahindi, kunde, nafaka kuu, mafuta ya mbogamboga na chumvi. Kwa sababu ya upungufu wa fedha, aina zote tano za vyakula kwa mwezi Agosti zinakidhi tu asilimia 62 ya kiasi cha kalori 2,100 zinazopendekezwa kitaalamu kutosha mahitaji ya mtu ya siku.

“Pasipo mwitikio wa haraka kutoka wa wahisani, itakuwa lazima kupunguza mgao kwani akiba ya chakula inapungua kwa kasi sana,” amesema Mwakilishi wa WFP Tanzania Michael Dunford.

Akishukuru kwa msaada waliokwishapokea Dunford ametolea wito wahisani kutoa fedha zaidi kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kimsaada.

Kadhalika WFP imeonya hatari za kupunguza mgao ikiwemo kusababisha utapiamlo na kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa.