Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makombora Sana’a yaua raia- OHCHR

Makombora Sana’a yaua raia- OHCHR

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema makombora yaliyorushwa kutoka angani siku ya Jumatano kwenye maeneo mawili tofauti mjini Sana’a Yemen, yamesababisha vifo vya raia 33 na wengine 25 wamejeruhiwa.

Watu walioshuhudia matukio hayo wameieleza ofisi hiyo kuwa makombora hayo yaliangushwa kwa nyakati mbili tofauti kati ya saa tisa na saa kumi na nusu alfajiri ambapo kombora la kwanza lilianguka kwenye kituo cha ukaguzi kinachodhibitiwa na wahouthi.

Kombora la pili lilianguka kwenye hoteli moja iliyo takribani meta 10 au 15 kutoka kituo hicho cha ukaguzi ambapo wakati wa shambulio kulikuwemo watu 67.

Liz Throssel ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Liz)

“Katika matukio yote haya, ambamo raia waliuawa au walijeruhiwa, watu walioshuhudia tukio wanasema hakukuwepo na onyo lolote la awali kuwa shambulio lingaliweza kutokea. Kulenga raia au vifaa vya raia kumepigwa marufuku kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu ambayo inauzia mashambulio yasiyochagua.”