Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhila wanayokumbana nayo watoto Syria hayatajiki- UNICEF

Madhila wanayokumbana nayo watoto Syria hayatajiki- UNICEF

Athari wanazopata watoto kutokana na vita vinavyoendelea nchini Syria ni za kusikitisha, amesema mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini humo Fran Equiza.

Equiza akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi baada ya ziara yake kwenye maeneo ya Areesha Eza,  Ein Issa na Mabrouka amesema ameshuhudia watoto waliopoteza makazi wakiwa matumaini yao ni msaada kutoka UNICEF pekee.

Amesema wamepitia mambo machungu, wakashuhudia ghasia kubwa, wakipoteza familia zao lakini bado wana matumaini.

Equiza ametolea mfano mtoto mmoja mkimbizi aliyekutana naye, Rawan, aliyekimbia Raqqa ambaye alimwambia: 'Awali tulikuwa tunacheza lakini baadaye kukaja giza.’

Kwa mujibu wa ripoti inazopokea UNICEF kutoka ndani ya mji wa Raqqa, maelfu ya watu wanaendelea kunaswa mjini humo huku wakiwa mstari wa makabiliano.

Wakati mashirika ya msaada wa kibinadamu yakishindwa kufikia maeneo hayo, mji huo umeachwa bila huduma muhimu. Watoto na familia hawana maji safi huku hifadhi ya chakula inamalizika.