Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wakaribisha ripoti kuhusu Rakhine

UM wakaribisha ripoti kuhusu Rakhine

Umoja wa Mataifa umekaribisha ripoti ya kina iliyotolewa leo an kamisheni ya ushauri kuhusu jimbo la Rakhine huko Myanmar ambalo waumini wa dini ya kiislamu wanakabiliwa na sintofahamu ya utaifa.

Ripoti hiyo ilitangazwa leo na mwenyekiti wa kamisheni  hiyo ya watu tisa, Kofi Annan ikisisitiza suala la uraia kwa wananchi na kutoa wito wa watu kuwa huru kutembea na serikali ipatie suluhu chanzo cha ghasia na mizozo ya kikabila.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari jijini New  York, Marekani amesema..

(Sauti ya Dujarric)

“Umoja wa Mataifa unatarajia kupitia mapendekezo ya ripoti hiyo. Na kwa sasa inatambua kwa mara nyingine tena umuhimu wa hatua ya serikali ya kuanzisha kamisheni hii na umuhimu wa mamlaka yake ya kuchambua hali za jamii zote jimboni Rakhine na mapendekezo kuelekea kuzuia mizozo, kuleta maridhiano, kujenga taasisi na kuweka fursa za maendeleo na huduma za usaidizi wa kibinadamu.”

Halikadhalika Bwana Dujarric amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia serikali ya Myanmar katika kutekeleza mapendekezo hayo kwa maslahi ya jamii zote jimboni Rakhine.

Jopo hilo liliundwa na serikali ya Myanmar mwaka jana na kupewa jukumu la kupendekeza jinsi serikali inaweza kuendeleza jimbo la Rakhine na kujenga maridhiano miongoni mwa wakazi wake ambao wamekuwa wakizozana kwa muda mrefu sasa.