Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufugaji wa bata badala ya kuku wapunguza majanga Vietnam- UNISDR

Ufugaji wa bata badala ya kuku wapunguza majanga Vietnam- UNISDR

Umoja wa Mataifa umesema ingawa majanga ya asili hugharimu serikali pesa nyingi bado kuna mikakati nafuu inayoweza kuepusha nchi kukabiliana au kuepusha hasara inayoweza kutokea.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na udhibiti wa majanga, UNISDR Robert Glasser amesema hayo akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa siku moja kabla ya kuanza kwa jukwaa la nne kuhusu udhibiti wa majanga huko Panama.

Ametoa mfano wa Vietnam ambayo kila mwaka hukumbwa na mafuriko kwenye mto Mekong akisema..

(Sauti ya Glasser)

“Wanavijiji hivi sasa wanafuga bata badala ya kuku, kwa sababu bata wanaelea na kuku hawaelei. Au wanajenga matuta ili yawalinde wakati wa mafuriko. Upunguzaji wa majanga unahitaji kuelewa hatari na kubuni mbinu ya utatuzi. Haimaanishi nyongeza ya mabilioni ya dola katika uwekezaji.”

Bwana Glasser amekumbusha kuwa mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yanategemea udhibiti wa majanga ambayo hukumba maeneo mbali mbali duniani kila uchao hivyo amesema..

(Sauti ya Glasser-2)

“Kujumuisha hatari za majanga kwenye SDGs na mipango ya kiuchumi ni jambo la msingi hivi sasa ili kuweza kusonga mbele kwa usahihi na ufanisi.”