Anti-Balaka na FPRC wapambana huko CAR

23 Agosti 2017

Huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSCA umeripoti mapigano hii leo kati ya wanamgambo wa kikundi cha Anti-Balaka na wale wa FPRC awali wakijulikana kama Seleka.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema mapigano hayo yametokea kwenye eneo la Ngubi, karibu na mji wa Bria jimboni Haute-Kotto.

Amesema walinda amani wa Umoja  wa Mataifa wanajaribu kuleta maelewano kati ya pande hizo, huku wakiweka doria kwenye kanisa ambamo kwao wakimbizi wa ndani wamesaka hifadhi.

Halikadhalika Bwana Dujarric amezungumzia kuhusu wakimbizi wa ndani waliokuwa wamesaka hifadhi kwenye kituo cha MINUSCA mjini Bria kufuatia mapigano ya hivi karibuni.

(Sauti ya Dujarric)

“Takribani raia 6,000 waliokuwa wamesaka hifadhi kwenye kituo cha Umoja wa Mataifa mwishoni mwa wiki wamerejea kwenye kituo cha kuhifadhi wakimbizi wa ndani mjini humo, kituo ambacho kinalindwa pia na walinda amani.”

Wakati huo huo, Bwana Dujarric amenukuu maafisa wa  haki za binadamu nchini CAR wakieleza wasiwasi kwamba ..

(Sauti ya Dujarric)

“Hali ya kibinadamu huko Zemio wakisema kuna uwekezano hali ikawa mbaya kufuatia kuwasili tarehe 21 mwezi huu kwa watu wa kabila la Fulani wakiwa na silaha nzito, sambamba na ripoti ya kwamba wapiganaji wa Anti-Balaka wanatoka Bengasu kuelekea Zemio.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter