Ukosefu wa uhakika wa chakula huchochea uhamiaji- Ripoti

23 Agosti 2017

Ripoti mpya ya utafiti wa pamoja wa mashirika mbali mbali ikiwemo lile la Mpango wa chakula duniani WFP , imebaini uhusiano uliopo kati ya ukame wa muda mrefu nchini El Salvador, Guatemala na Honduras uliochochewa na El Niño ya kuanzia mwaka 2014 hadi 2016 na kuongezeka kwa wahamiaji kutoka nchi hizo kuelekea Marekani.

Akizungumzia ripoti hiyo iliyozinduliwa leo ikiwa na maudhui  “Uhakika wa chakula na uhamiaji: Kwa nini watu hukimbia na athari kwa familia wanaosalia El Salvador, Guatemala, na Honduras”, Mkurugenzi Mkuu wa WFP kanda ya Amerika ya Kusini, na visiwa vya Caribbea Miguel Barreto, amesema ripoti inatoa picha halisi ya sababu za watu kuhama.

(Sauti ya Miguel)

“Tunaonyesha kuna changamoto kati ya uhakika wa chakula na uhamiaji, lakini pia watu wengi wanaosalia, familia za wahamiaji wanaathirika.  Lengo la utafiti ni kuhimiza umuhimu wa uwekezaji wa programu za muda mrefu ili kuzuia watu zaidi kuhama.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo familia za wahamiaji huachwa na mzigo wa kulipa deni la waliohama na iwapo safari za wahamiaji hazifanikiwi basi deni huwa kubwa zaidi na mahitaji ya chakula hayatoshelezwi.

Asilimia 78 ya familia za wahamiaji hutegemea hela zinazotumwa kutoka nje huku asilimia 42 waliohojiwa wakisema fedha hizo ndizo kipato pekee cha familia.

Fedha hizo hutumika kwa mahitaji ya chakula, kuwekeza kwenye kilimo na kuanzisha biashara ndogo ndogo.