Waathirika wa ubakaji wa ISIL lazima wapate msaada unaohitajika-UM

22 Agosti 2017

Leo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq UNAMI wametoa ripoti ikiitaka serikali ya Iraq kuhakikisha kwamba maelfu ya wanawake na wasichana manusura wa ubakaji na mifumo mingine ya ukatili wa kingono ulioteklelezwa na kundi la ISIL wanapata huduma, ulinzi, na haki na kwamba watoto waliozaliwa kutokana na ukatili huo hawatakuwa na maisha ya ubaguzi na unyanyasaji.

Ripoti inasema wanawake na wasichana kutoka katika maeneo yanayodhibitiwa na ISIL hususani wa jamii ya Yezidi na jamii zingine za walio wachache wamekuwa katika hatari ya ukiukwaji wa haki za binadamu na sharia za kimataifa ikiwemo ubakaji na ukatili, kutawanywa kwa lazima, kutekwa, kunyimwa uhuru, utumwa, kulazimishwa kubadili dini, kufanyiwa unyama, vitendo visivyo vya kiutu na kudhalilishwa.

Kamishina mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra'ad Al Hussein amesema majeraha hayo ya kimwili, kiakili na kihisia yaliyosababishwa na ISIL ni ya kupindukia na ili waathirika waweze kujenga upya Maisha yao na watoto wao wanahitaji haki na hatua. Liz Throssell ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Geneva

(SAUTI YA LIZ)

"Serikali ya Iraq ina wajibu wa chini ya sharia za kitaifa na za kimataifa kuhakikisha waathirika wote wana fursa ya kupata haki na fidia. Wajibu huu ni pamoja na kuhakikisha uwajibikaji wa wanaodaiwa kuhusika kupitia kesi mbele ya mahakama huru zitakazoendeshwa kwa kuzingatia unyeti wa suala la jinsia ili kutotonesha vidonda vya waathirika.”

Ripoti pia imeelezea kutambua juhudi zilizofanywa na serikali na jimbo la Kurdistan kuchagiza haki za wanawake na watoto na kushughulikia mahitaji waathirika wa ISIL.