Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa EU kwa WFP kupunguza machungu kwa wakimbizi Algeria

Msaada wa EU kwa WFP kupunguza machungu kwa wakimbizi Algeria

Muungano wa Ulaya, EU umelipatia shirika la mpango wa chakula duniani, WFP msaada wa dola milioni 5.5 kwa ajili ya mahitaji muhimu ya chakula kwa wakimbizi wa Sahrawi walioko kwenye kambi nchini Algeria.

Kupitia fedha hizo wakimbizi watakuwa na uhakika wa mlo ambapo watapatiwa nafaka, mafuta, sukari na vyakula vilivyoongezewa virutubisho.

Mwakilishi wa WFP nchini Algeria Romain Sirois amesema fedha hizo zimekuja wakati muafka kwa kuwa wakimbizi hao wamekuwa wanategemea usaidizi kwa zaidi ya miaka 40, wakiishi kwenye mazingira magumu kwenye jangwa la Sahara.

Muungano wa Ulaya ni moja ya wahisani wakuu wa WFP ambapo mwaka huu pekee msaada wao ni karibu theluthi moja ya mahitaji ya WFP kwenye ukanda huo wa kaskazini.