Zeid apongeza kufutwa kwa sheria zinazolinda wabakaji

22 Agosti 2017

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein amekaribisha kitendo cha Lebanon, Tunisia na Jordan kufutilia mbali sheria ambazo zinalinda wabakaji dhidi ya mashtaka kwa kuwaruhusu kuwaoa wale waliowabaka.

(Taarifa ya Assumpta)

Zeid amesema kitendo cha wabunge katika nchi hizo kufuta sheria hizo kinadhihirisha azma yao ya kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake.

Amesema kumuadhibu mtu aliyebakwa kwa kumuoza kwa mtu aliyembaka ni uhalifu mkubwa dhidi yake na hauna nafasi katika zama za sasa.

Kamishna Zeid ametaja uamuzi huo kuwa ni ushindi mkubwa akipongeza kampeni za miaka kadhaa zilizoendeshwa na watetezi wa haki za binadamu hususan wanawake huko Tunisia, Lebanon na Jordan.

Ametoa wito kwa serikali na wananchi kwenye nchi zilizo ukanda wa mashariki ya kati na kwingineko kuiga mfano huo ili kufuta sheria zinazolinda ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana.