Idadi ya watoto wanaojilipua Nigeria yaongezeka- UNICEF

22 Agosti 2017

Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF limeeleza masikitiko yake kufuatia ongezeko la watoto wanaotumiwa kwenye mashambulizi ya kujilipua huko kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

(Taarifa ya Kibego)

Msemaji wa UNICEF huko Geneva, Uswisi Christophe Boulierac amesema katika kipindi cha mwaka mmoja idadi imeongezeka mara nne.

Bwana Boulierac amesema kitendo cha kutumia watoto ni mauaji na kwamba wao si watekelezaji bali ni wahanga wakuu kwa kuwa wanatumiwa na watu wazima kwenye mashambulizi hayo ambayo mara nyingi magaidi wa Boko Haram wamekiri kuhusika.

(Sauti ya Boulierac)

“Kuna watoto 83 ambao wametumiwa kwenye mashambulizi ya kujilipua tangu tarehe mosi Januari mwaka huu wa 2017. Kati ya hao wanaojilipua 55 ni wasichana na wengi wao wana umri wa chini ya miaka 15. Kuna wavulana 27, halikadhalika kuliwepo pia na mtoto mchanga.”

UNICEF imesema inashirikiana na mamlaka nchini Nigeria ili kuepusha watoto kujikuta katika mazingira yanayoweza kuwatumbukiza kwenye vitendo hivyo vya kubeba mabomu na kujilipua.