Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO yatangaza jopo la wataalam kwa mustakbali bora wa ajira

ILO yatangaza jopo la wataalam kwa mustakbali bora wa ajira

Shirika la kazi ulimwenguni ILO, limetangaza leo kuanzishwa kwa tume ya ngazi ya juu ya kimataifa ya wataalamu 20 ambayo itaangalia taasisi, usimamizi na sheria zinazohitajika ili kuhakikisha ajira zinakidhi viwango vya kisheria ikiwa ni juhudi za ILO katika mikakati ya mustakabali wa kazi zilizoasisiwa na shirika hilo mwaka 2013.

Akizungumza katika tukio la uzinduzi wa jopo hilo mjini Geneva Uswisi mkurugenzi mkuu wa ILO Guy Ryder, amesema wataalamu hao wanawakilisha taswira ya ulimwengu kwani wamezingatia misingi ya kanda wanakotoka, jinsia, ni waajiriwa au waajiri na hivyo wanamatumaini makubwa wakati wakianza utekelezaji wa jukumu lao.

Bwana Ryder ameongeza kwamba wakati wataalam hao wakiangazia maswala mbali mbali pia..

“Watagusia maswala muhimu ya nyakati za sasa, maswala yanayozungumziwa kwenye vyombo vya habari kila uchao, maswala yanayojitokeza kisiasa katika nchi wanachama na maswala ambayo kwa kawaida ni kielelezo cha matumaini au wasiwasi wa familia kote ulimwenguni.”

Wataalamu katika tume hiyo wataandaa ripoti huru ambayo itawasilishwa kwenye mkutano wa maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa ILO mwaka 2019.

Miongoni mwa walioshuhudia kutangazwa kwa tume hiyo ni pamoja na wenyeviti wenza wa tume hiyo Rais wa Mauritius Ameenah Gurib-Fakim na Waziri Mkuu wa Sweden Stefan Löfven.