Wahisani angazieni pia elimu Pembe ya Afrika

21 Agosti 2017

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yametoa wito kwa wahisani kufadhili kwa kina mahitaji ya elimu kwa nchi zenye mahitaji ya kibinadamu katika pembe ya Afrika. Flora Nducha na taarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA)

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la watoto UNICEF wamesema katika taarifa yao kuwa elimu ikienda sambamba na usaidizi wa kibinadamu ni muhimu katika kuleta maendeleo kwa nchi hizo zinazokabiliwa na ukame ambazo ni Ethiopia, Somalia na Kenya.

Wamesema ufadhili utumie shule na maeneo ya kujifunzia kama majukwaa salama na jumuishi ya kupitisha misaada ya dharura na ya kawaida huku serikali nazo zikitakiwa zihakikishe watoto na vijana waliohama makazi yao wanapata elimu popote pale walipo kwa kuzingatia ajenda 2030 inayoainisha haki ya elimu kwa watoto wote.

Ukame unatishia mustakhbali wa watoto na vijana huko Ethiopia, Somalia na Kenya ambapo ufadhili unaotakiwa wa dola bilioni 2.7 umechangiwa dola milioni 970 tu, sekta ya elimu ikiambulia asilimia 1.7.