Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wasigeuzwe ngao au silaha kwenye mizozo

Raia wasigeuzwe ngao au silaha kwenye mizozo

Leo ni siku ya usaidizi wa kibinadamu duniani ambapo suala la msingi linalopatiwa kipaumbele ni usalama kwenye maeneo yenye vita, wakiangaziwa raia na wale wanaowapatia misaada.

Umoja wa Mataifa unasema mamilioni ya watu hivi sasa wanaishi kwenye maeneo yenye mizozo, wakiwemo watoto, wanawake na wanaume.

Taswira ya miji yao awali ikiwa na huduma za msingi kama vile masoko, bustani, maduka, shule, hospitali, viwanda na viwanja vya michezo imegeuka na kuwa uwanja wa vita.

image
Picha:UNHCR/Ivor Prickett (file)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema kupitia ujumbe wake wa siku hii kuwa baada ya maeneo hayo kugeuzwa uwanja wa vita, raia wanakosa huduma za msingi na wanaishi Maisha ya hofu.

Na kama hiyo haitoshi, wanawake na wasichana wanakuwa hatarini kukumbwa na ukatili wa kingono, ilhali watoto wengine wakitumikishwa kwenye makundi yenye silaha.

Na kwa wale ambao wanataka kupeleka misaada kwa makundi hayo, hali inakuwa ngumu kwani wanakabiliwa na mashmbulizi kutoka pande kinzani za mzozo husika.

Kwa mantiki hiyo, Umoja wa Mataifa kupitia ofisi yake inayoratibu misaada ya kibidamu imezindua kampeni iitwayo Rais si Walengwa #NotATarget, kampeni inayotekelezwa kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandano ili kuhamasisha jamii kuchukua hatua.

Hatua hizo kwa mujibu wa tovuti maalum ya kampeni hiyo www.worldhumanitarianday.org ni pamoja na pande kinzani kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na kuhakikisha raia hawageuzwi ngao au silaha kwenye mapigano.