Hatma ya amani ya Yemen bado iko njia panda:Ould Cheikh

18 Agosti 2017

Hatima ya amani ya Yemen bado iko njia panda huku machafuko yakiendelea kushuhudiwa katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo ikiwemo mji mkuu Sa’ana.

Akiwasilisha tarifa ya tathimini ya mchakato wa amani ya Yemen kwenye baraza la usalama hii leo mjini New York Marekani, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed amesema katika miezi michache iliyopita hali ya machafuko imeongezeka na gharama kubwa inabebwa na raia.

Amesema raia Taiz wanaendelea kuathirika na mashambulizi ya makombora katika makazi ya watu na mapigano na mashambulizi ya anga pia yameongezeka katika eneo la Pwani kufuatia kuzinduliwa kwa operesheni ya Golden spear na serikali ya Yemen na majeshi washirika, pande zote zimeendelea kudai kupiga hatua kubwa katika vyombo vya habari lakini bado anaamini kwamba hakuna uwezekano wa suluhu ya kijeshi. Kupitia sauti ya mtafsiri bwana Cheikh amesema

(SAUTI YA CHEIKH)

“Tunashuhudia mashambulizi kila siku , na upande mwingine kujibu mashambulizi hayo, wale wanaosaka suluhu ya kijeshi wataendelea kuongeza madhila yaliyosababishwa na vita na kuruhusu tishio la ugaidi kuendelea kupanua wigo na pia kuongeza changamoto za Yemen kujaribu kujikwamua baada ya vita.”