Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunashikamana na Hispania kufuatia shambulio la Barcelona:UM

Tunashikamana na Hispania kufuatia shambulio la Barcelona:UM

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali shambulio la kigaidi mjini Barcelona Hispania lililokatili maisha ya watu 13 na kujeruhi wengine zaidi ya 100. Shambulio hilo lilitokea Alhamisi kwenye wilaya ya Las Ramblas iliyo maarufu kwa watalii katikati ya mji wa Barcelona.

Baraza limetoa tarifa ya kusisitiza kwamba vitendo vyovyote vya kigaidi ni uhalifu usiohalalishwa , bila kujali sababu yoyote ya kuvitekeleza.

Wajumbe 15 wa baraza hilo wamehimiza haja ya kuwafikisha wahusika, wafadhili na watekelezaji kwenye mkono wa sheria kwa kile walichokielezea kama vitendo vya kinyama.

Wajumbe hao pia wamesema wanashikamana na serikali na watu wa Hispania na kutoa wito wa juhudi za kimataifa katika kukabiliana na ugaidi na itikadi kali.