Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Al Mahdi kulipa fidia ya zaidi ya dola milioni 3 kwa uharibifu Timbuktu

Al Mahdi kulipa fidia ya zaidi ya dola milioni 3 kwa uharibifu Timbuktu

Hii leo mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague, Uholanzi imemtaka Ahmad Al Faqi Al Mahdi anayetumikia kifungo cha miaka 9 kwa makosa ya uhalifu wa kivita huko Timbuktu, Mali alipe fidia ya zaidi ya dola milioni 3.

Mahakama hiyo imesema fidia hiyo ni kwa ajili ya watu na jamii ya Timbuktu kufuatia mashambulizi ya makusudi aliyofanya dhidi ya majengo ya kidini na kihistoria mjini humo.

Kwa kutambua kuwa Al Mahdi hivi sasa hana uwezo, ICC imehimiza mfuko wa fidia kwa wahanga, TFV ukidhi mahitaji hayo ya fidia na kuwasilisha mbele ya mahakama hiyo mpango wa utekelezaji tarehe 16 Februari mwakani.

Fidia inalenga ukarabati wa majengo na pia uwezeshaji wa watu waliokuwa wanategemea majengo hayo ya kihistoria ili kujipatia kipato, lakini pia watu ambao makaburi ya jamaa zao yaliharibiwa wakati wa mashambulizi hayo.

Upande wa utetezi una haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30 kuanzia leo.