Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchele uliorutubishwa unaweza kabili ukosefu wa damu- Tafiti

Mchele uliorutubishwa unaweza kabili ukosefu wa damu- Tafiti

Utafiti mpya umebaini kuwa ulaji wa mchele ulioongezewa virutubisho unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa damu na uhaba wa madini ya Zinki mwilini.

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema utafiti huo ulihusisha wanawake maskini zaidi huko Bangladesh ambao walipatiwa mchele huo kupitia mpango wa maendeleo wa serikali kwa watu walio hatarini zaidi, VGD.

Kupitia mpango huo, wanawake hao pamoja na kupatiwa kilo 30 za mchele uliorutubishwa, walipatiwa pia dola 185 kila mmoja kama mkopo wa riba nafuu ili kuinua vipato vyao.

Kiwango cha upungufu wa damu kilipungua kwa asilimia 4.8 ilhali uhaba wa madini ya Zinki ulipungua kwa asilimia 6 miongoni mwa wanawake hao.

Mwakilishi wa WFP nchini Bangladesh, Christa Räder, amesema kupitia utafiti huo wamebaini mbinu za kujumuisha mgao wa mchele huo kupitia mpango wa serikali na wakati huohuo kuboresha hali ya lishe na kipato kwa wanawake.